TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ina pambana kwa hali na mali kuhakikisha adui rushwa anatoweka, kwani ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo, utendaji mzuri na haki.
Juhudi hizo zinapaswa kupata ushirikiano wa kutosha ikiwAmo kuweka mazingira mazuri ya kuweza kuzuia vitu vinavyoshawishi rushwa.
Mazingira ya kuzuia rushwa yanawekwa na kila mmoja katika nafasi yake ya kazi kwani rushwa inapenya kila mahali, watoaji na wapokeaji wanapatikana pia katika maeneo hayo.
Kuna mazingira mengi yanayoweza kushawishi rushwa lakini kwa leo ningependa kuzungumzia kwa upande wa Jeshi la Polisi ambalo linakabiliwa na tatizo hilo kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Malalamiko ya rushwa kwa jeshi hilo yanaonekana kuwa ya kweli kwani kuna Polisi kadhaa ambao walifukuzwa kazi kutokana na kashfa hiyo.
Vitendo vya rushwa vimelitikisa Jeshi la Polisi nchini kwani kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni mwaka huu, askari 68 walifukuzwa kazi huku kesi nyingine tisa za makosa ya jinai zikiendelea mahakamani.
Taarifa hizo zilithibitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Anasema Jeshi la Polisi limeendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wake wanaojihusisha na vitendo vya rushwa. Katika mwaka wa 2011/12, jumla ya malalamiko 625 ya wananchi dhidi ya kero za rushwa yalishughulikiwa.
Ili kuhakikisha rushwa inapungua kama si kumalizika katika jeshi wameanzisha utaratibu wa kuwazawadia askari wanaokataa kupokea rushwa katika utendaji wao wa kazi.
Juhudi zote hizo zinafanyika kwa nia nzuri lakini tunasahau kwamba yapo mazingira mabovu katika baadhi ya vituo vya polisi na maeneo jirani ya vituo yanayoshawishi upokeaji wa rushwa na utoaji.
Siwezi kutaja vituo vyote lakini ningependa kutolea mfano Kituo cha Polisi Buguruni, ambacho kina biashara ya vinywaji mbalimbali zikiwamo bia.
Polisi Buguruni kuna maeneo mawili mbele ya eneo wanalopumzika wananchi waliofika kufuatilia ndugu zao au wenye shida kituoni hapo, eneo moja linafanya biashara ya vinywaji baridi soda, juisi na vyakula na lingine linauza vilevi mbalimbali zikiwamo bia aina zote zinazozalishwa na viwanda vyetu nchini.
Nasikitika sana kuyaona mazingira hayo katika kituo kikubwa kama hicho, najua polisi huwa wanapata muda wa kukaa katika maeneo yenye vilevi na hata vinywaji hivyo huuziwa kwa gharama ya chini katika maduka yao ukilinganisha na maeneo mengine ya uraiani.
Lakini kwa nini vinywaji hivyo viuzwe muda wa kazi bila kudhibitiwa, hakuna mwananchi anayeweza kufika eneo lile akabaini kwamba askari aliyeshikilia chupa ya kinywaji cha kilimanjario bia alishamaliza zamu anatakiwa kurudi nyumbani ndio sababu analewa.
Tunaamini askari waliopo kituoni muda wa kazi wako kazini hivyo hawaruhusiwi kulewa wawapo kazini, ni jambo la aibu na linaloshawishi vitendo vya rushwa.
Mtakubaliana na mimi kwamba mlevi hawezi kuona bia akakosa kuitamani na kama hana fedha basi atafanya kila jitihada kuhakikisha anapata fedha za kununua hata bia mbili.
Polisi asiye na fedha na mlevi atawezaje kujizuia katika mazingira kama hayo kama hatojiingiza katika mipango haramu ya kutisha ndugu wa mtuhumiwa ili wampe fedha akalewe na kujifanya katoa msaada wa kumwachia kumbe ilikuwa ni haki yake.
Nimeshuhudia matukio hayo katika grosary ya Buguruni, nimekaa kwa saa zaidi ya tano kuanzia saa tano asubuhi hadi kumi na moja jioni eneo hilo nikiwashuhudia Polisi wanaotoka humo, wengine walikuwa na chupa za bia, wengine wametulia wanakunywa kana kwamba wako katika mazingira salama ya kunywa pombe.
Mbali na Buguruni vipo vituo vya Polisi ambavyo pembeni yake kuna grosary ambapo vitendo ni hivyo hivyo na wakati mwingine mwenye shida anaweza kumfuata Polisi katika kiti kirefu. Haipendezi inadhalilisha jeshi.
Katika mazingira hayo ndio sababu unaweza kupata tatizo usiku na kuwafata Polisi, katika gari lao utakaowakuta hawakulewa ni wachache wengine wote wako chakari, wanawezaje kufanya kazi, wenyewe ndio wanajua.
Mwananchi akikuona wewe ni cha pombe anajua akikutangazia rushwa lazima utapokea na kumwachia hata kama ni mhalifu hatari aliyeistahili kuchukuliwa hatua ili kukomesha maovu anayofanya.
Pia kwa tamaa zako za kupata fedha za kununulia pombe unaweza kumnyima au kumcheleweshea raia haki yake ili mradi tu ashawishike kutoa fedha, si za kuhudumia familia bali kulewea.
Inawezekana mazingira hayo yanaonwa na wakubwa lakini viongozi kaeni chini mtafakari mtawezaje kukomesha rushwa wakati kuna mazingira yanayoshawishi kupokea rushwa vituoni au jirani na vituo vya polisi?
Kinachostahili kuwepo katika vituo vya Polisi ni soda, maji, juisi na si vilevi kwani pamoja na kushawishi rushwa pia ni hatari pale mtu anapolewa, akakereka na jambo anaweza kumdhuru aliyemkera.
Mfano mwananchi kashawishiwa kutoa rushwa, akatoa na malengo yake yakachelewa kutimia au hayakutimia kabisa atashindwa nini kunywa pombe nyingi na kumfanyia fujo aliyechukua fedha yake bila kumsaidia.
Si kila mmoja anaweza kujizuia anapokuwa kalewa, wapo wanaolewa jambo la kwanza ni kutafuta wa kuchokoza ili wapigane, hamuoni kuweka vilevi katika maeneo hayo inahatarisha usalama wa kituo cha polisi na watendaji.
Kama haiwezekani kuondoa grosary hizo katika maeneo hayo uwekwe utaratibu wa kuwadhibiti Polisi katika unywaji wa pombe muda wa kazi, haiwezekani raia mitaani wakikutwa baa wanakunywa bia muda wa kazi wakamatwe wakati Polisi wanalewa muda wa kazi.
Acheni kuwaonea raia, kama ni sheria inakataza kunywa pombe muda wa kazi basi sheria hiyo ifanye kazi pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment