Kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Msalato, Mkoa wa Dodoma zimezidi kupamba moto, huku Chadema na CCM vikionyesha kuchuana vikali.
Hali hiyo imesababisha kuwapo kwa vituko na vitimbwi kadhaa hasa imani zinazohusiana na masuala ya ushirikina.
Imani za ushirikina zilibainika juzi baada ya bundi kukutwa chumbani kwa mgombea udiwani wa Chadema, Nsubi Bukuku ilhali hakuna tundu lolote chumbani au nyumba linalowezesha ndege mkubwa kama bundi kuindia.
“Hatukatai kuwa huyu ni ndege kama walivyo ndege wengine, lakini kwa imani zetu Waafrika ndege huyu ni nadra kuingia chumbani kwa mtu na mara nyingi hutumiwa kwa masuala ya ushirikina,” amesema Alphonce Mawazo ambaye ni Meneja wa kampeni.
“Kwa hiyo tunaamini sasa wenzetu CCM Msalato, sera zimewashinda wameingia kwenye masuala ya ushirikina.”
Licha ya tukio hilo, kampeni hizo zimeshuhudia kuwapo kwa mbinu mpya ya kusambaratisha wafuasi wanaosikiliza mikutano ya kampeni, nyuki wamekuwa wakiwekwa katika mifuko ya plastiki na kufunguliwa katikati ya kundi la watu, hali ambayo husababisha watu kukimbia.
Tukio hilo lilitokea Kitongoji cha Chikowo, Chadema walipokuwa wakimnadi mgombea wao ghafla vijana ambao hawakufahamika aliyewatuma, walifungulia nyuki ambao waliwashambulia watu hao.
“Walianza vipigo wameona tunaendelea kuvumilia,watu wanazikubali sera zetu na kumkubali mgombea wetu,sasa wameanza kutumia mbinu chafu zaidi ushirikina na Nyuki,lakini nataka kusema mbinu zote hizo zimeshindwa maana tuna hakika tarehe Novemba 4, Kata ya Msalato itakuwa chini ya Chadema,”alisema Mawazo.
Kwa upande wake, Bukuku amesema vitibwi vinavyofanywa na wapinzani wake, haviwezi kurudisha harakati zake za kutaka kuikomboa kata hiyo ambayo haina zahanati tangu uhuru.
No comments:
Post a Comment