Feb 13, 2013

TAMKO LA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM KUHUSU MAANDAMANO NA VURUGU ZILIZOTOKEA MKOANI MTWARA JUU YA UJENZI WA BOMBA LA GESI NA MAENDELEO YA MKOA WA MTWARA


Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti ,Makao Makuu ya CCM ,Dodoma leo tarehe 13/2/2013. 

1.       Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea maelezo ya Serikali kuhusu maandamano na vurugu zilizotokea Mkoani Mtwara tarehe 27 Desemba, 2012 tarehe 25 Januari, 2013 na tarehe 26 Januari, 2013. Maandamano na vurugu hizo zilizodaiwa kuwa na lengo la kupinga mradi wa bomba la Gesi kujengwa na kupeleka Gesi Dar es Salaam.

2.       Baada ya kupokea maelezo haya ya Serikali, Halmashauri Kuu ya Taifa imebaini kuwa: -

(a)           Kwa sehemu kubwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara hawakuwa wamepewa elimu ya kutosha juu ya uendelezaji wa Gesi na jinsi watakavyonufaika.

(b)           Baadhi ya Wanasiasa na baadhi ya Viongozi wa Makundi mbalimbali waliamua kutomia suala la Gesi kupandikiza lugha za chuki, uchochezi na upotoshaji wa maendeleo ya Mradi wa Gesi kwa lengo la kujitafutia umaarufu.

(c)            Suala la Gesi limetumika kama kisingizio tu cha kufanya vitendo vya rurugu na uvunjifu wa amani.



3.       Kutokana na ukweli huu, Halmashauri Kuu ya Taifa inaelekeza ifuatavyo:-

(i)             Imesikitishwa na vurugu zilizotokea na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na uharibifu mkubwa wa mali  na majengo  ya CCM, Serikali, Wabunge na watu binafsi. Halmashauri Kuu ya Taifa inawapa pole wafiwa na waliopoteza mali zao.

(ii)      Inaiagiza Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu waliofanya vurugu na uharibifu mbalimbali na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria. Pia, kuwa makini na kuhakikisha matukio kama haya hayajitokezi tena.

(iii)        Inaiagiza Serikali kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi wa maeneo husika  kuhusishwa na kuelimishwa juu ya miradi mbalimbali kwenye maeneo yao.

(iv)        Halmashauri Kuu ya Taifa inawataka Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo desturi yao, maana vurugu pamoja na kuharibu mali na kugharimu maisha  vinaweza kuwakimbiza wawekezaji waliojitokeza na ambao  shughuli zao zitawafaidisha  wananchi wa Mkoa huu na Watanzania kwa ujumla .

No comments:

Post a Comment