Jul 23, 2012

WANAWAKE NA WATOTO WANYANYASIKA KIJINSIA TANZANIA...

ZAIDI ya wanawake 5, 000 hapa nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kinyama vinavyoambatana na ukatili wa kijinsia, kila mwaka. Takwimu hizo zilitolewa juzi na Mwakilishi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hapa nchini, Onesmo Ngulumwa, alipokuwa akizungumza wakati wa kutengeneza kipindi kinachozungumzia ukatili wa kijinsia na watoto. Kipindi hicho kinajulikana kama Zungumza na kinaendeshwa na Mradi wa Sera ya Afya, kwa hisani ya Shirika la Futures Group, Internatinal na kufadhiliwa na USID kupitia Mfuko wa dharura wa Rais wa Mpango wa Ukimwi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Ngulumwa alisema unyanyasaji wa kijinsia unaendelea kukithiri hapa nchini na kusababisha wanawake na watoto kuishi maisha ya kuteseka. "Orodha ya ukatili ni mkubwa mno hapa nchini, waathirika wakubwa wa unyanyasaji huu ni wanawake na watoto wanaofanyiwa ukatili ikiwa ni pamoja na kubakwa, kukeketwa na ukatili mwingine mwingi unaofanyika kwenye jamii zetu," alisema Ngulumwa. Mshahuri Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano, Vijana na Vyombo vya Habari katika mradi huo, Asha Mtwangi, alisema lengo la kipindi hicho ni kuelimisha jamii juu ya unyanyasaji wa kijinsia. "Katika kipindi hiki viongozi wa dini watazungumza ni namna ya dini na zinasaidiaje kuelimisha jamii yetu juu ya ukatili huo wa kijinsia," alisema Asha. Alisema mbali na kipindi hicho, mradi pia umezindua sera na muungozo kuhusu  ukatili wa kijinsia na afya ya jamii. Asha alisema kipindi hicho kitaangalia namna jamii inavyoathirika na tatizo la ukatili wa kijinsia na namna wanawake na watoto wanavyoathirika kisaikolojia baada ya kufanyiwa ukatili huo.

No comments:

Post a Comment