Aug 9, 2012

SIASA LEO...

RAIS KIKWETE ALIVYOMFUNGA MDOMO MEMBE




ALISEMA ANGEWATAJA WATUHUMIWA, RAIS AKASEMA HAKUNA USHAHIDI, WABUNGE WAPINGA MJADALA KUFUNGWA, WASEMA WAHUSIKA WAPO, WASHTAKIWE.

KAULI iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba hakuna ushahidi wa kuwashtaki watuhumiwa rushwa ya rada, inaonekana kumfunga mdomo Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye aliwahi kuahidi kwamba angewataja watuhumiwa hao.

Rais Kikwete alipokutana na wakuu wa vyombo vya habari wiki iliyopita, alisema Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo kutokana ukweli kwamba hata Uingereza walikana Kampuni ya BAE Systems kutoa rushwa na badala yake wakasema ilikosea katika kuandika hesabu zake.

Wakati Rais Kikwete akisema hakuna ushahidi wa kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa ya rada, tayari Membe alikuwa amesema watuhumiwa wapo, anawajua na aliahidi kwamba angewataja bungeni.

Hata hivyo, Membe aliyewasilisha Hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya wizara yake bungeni juzi, alishindwa kutekeleza ahadi yake licha ya kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wabunge, wakiongozwa na Waziri Kivuli wa wizara hiyo, Ezekia Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana (Chadema).

Juzi, kabla Membe hajasoma hotuba yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alitoa taarifa rasmi ya Serikali bungeni kuhusu suala hilo na alisema kuwa, hakuna mtuhumiwa wa rada anayeweza kupelekwa mahakamani na kutamka kwamba mjadala kuhusu suala hilo umefungwa rasmi.

“Hata Uingereza iliyochunguza suala hilo imeeleza bayana kwamba hakuna rushwa na katika hatua hiyo, Serikali haiwezi kumfikisha mtu yeyote mahakamani,” alisema Chikawe.

Kauli hiyo ya Serikali inaonekana kuwakera baadhi ya wabunge ambao jana waliliambia gazeti hili kwamba wanashangazwa na jinsi Serikali ilivyomaliza na kufunga mjadala wa ufisadi wa rada, hali kukiwa na kila dalili kwamba wapo Watanzania waliohusika katika ufisadi huo.

Kauli za wabunge
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema: “Ushahidi wa kwanza ni fedha zilizorejeshwa kwa sababu Watanzania walilipa zaidi. Kama kuna fedha zililipwa zaidi, iweje asipatikane mtu wa kuchukuliwa hatua. Tulivyoelezwa ni kuwa vyombo vya uchunguzi vilikuwa vinachunguza suala hili, sasa tunashangaa kuelezwa kuwa hakuna uchunguzi unaoendelea.”
Alihoji kama fedha zaidi ya Sh70 bilioni zililipwa zaidi, kwa nini waliohusika na uzembe huo wasichukuliwe hatua?

Alisema kama fedha za nchi zimelipwa zaidi,
inawezekana kulikuwa na ufisadi au uzembe na hayo yote yanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangala alisema kuwa, amefurahishwa na msimamo wa mawaziri katika suala hilo ingawa haamini kama ungekosekana ushahidi wa kumnasa aliyehusika.

“Siamini kama ilishindikana kupata ushahidi, ninachokiona ni kwamba hakukuwa na juhu
di za kuhakikisha unapatikana ushahidi na wahusika waliamua jambo hili liende kama lilivyo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema atamwandikia rasmi Spika kwa mujibu wa Kanuni ya 46 ili waziri atakiwe kujibu kwa ukweli na kuacha kutetea ukiukwaji wa sheria.

Alisema Waziri Chikawe alitoa taarifa potofu kuwa makubaliano yaliyoidhinishwa na Mahakama ya Uingereza Desemba 21, 2010 yanaifanya Serikali ya Tanzania ishindwe kuchukua hatua za kisheria dhidi ya ufisadi huo, akisema wakati ripoti ya Kamati ya Bunge la Uingereza ya
Maendeleo ya Kimataifa kuhusu uchunguzi wa uhalifu wa fedha ya Novemba 14, 2011 ilisisitiza wahalifu wa ufisadi huo wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia alisema madai ya waziri huyo kuwa Serikali ya Uingereza haikuwa tayari kutoa ushahidi na ushirikiano, hayana ukweli kwa akirejea msimamo wa Serikali hiyo uliotolewa Agosti 6, 2012.
Mbunge huyo alisema Waziri Chikawe hakujibu kikamilifu swali lake la jana asubuhi pale alipohoji kwa nini Serikali isichukue hatua za kisheria dhidi ya uzembe, matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na kuisababishia hasara Serikali kama ilivyofanya kwa mawaziri na watendaji wa Serikali waliofikishwa mahakamani kuhusu tuhuma hizo.

“Bila hata kupelekewa ushahidi wa rushwa anaodai waziri, mazingira ya mashtaka dhidi ya madai hayo na mengine ya ukiukwaji wa sheria yapo kwenye ripoti za Serikali yenyewe za nyakati mbalimbali,” alisema.

Mnyika alisema Serikali isipotangaza kuendelea na uchunguzi na kufungua mashtaka itabainika kuna ubaguzi katika uchukuaji wa hatua na mafisadi wakubwa wanalindwa.
Kutokana na msimamo wa Serikali ya Uingereza, Mnyika alimtaka Rais Kikwete kurekebisha majibu yake aliyoyatoa kwa wahariri na kuagiza vyombo vya dola viendelee kuchukua hatua.


Kauli ya JK Ikulu
Utata kuhusu suala hilo ulianza kuibuliwa na Rais Kikwete aliposema Ikulu kwamba Serikali imeshindwa kuwafungulia watu mashtaka ya rada kutokana na kukosekana ushahidi ambao ulitarajiwa kutoka Uingereza.

Alisema Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo kutokana na mazingira yaliyojengwa nchini Uingereza yakionyesha kwamba Tanzania haiwezi kupata ushahidi wowote kuhusu suala hilo.

“Sasa hapo sisi tunaanzia wapi, maana kwenye asili ya tukio hili, wanasema hakuna rushwa, kwa hiyo wanasheria wetu tukiwauliza nao wanahoji kwamba tunaanzia wapi katika suala hili,” alisema Kikwete.

Mara kwa mara Membe amenukuliwa akisema baada ya Serikali kupata chenji ya rada, lazima ijisafishe kwa kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa mahakamani. Membe alisema watuhumiwa wa rada wapo na lazima Serikali ijisafishe kwa kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria.
Juni mwaka huu, Membe alisema akiona kimya kinazidi kuhusu watuhumiwa wa rushwa katika kashfa ya rada, atawataja bungeni.

Alinukuliwa akisema kila aliyehusika na biashara hiyo ya rada ametajwa na kuwekwa picha yake katika kitabu cha, ‘The Shadow World-Inside the Global Arms Trade,’ kilichoandikwa na mwandishi wa Afrika Kusini, Andrew Feinstein.

Alisema atawataja kwa sababu kimya chao tangu kutoka kwa kitabu hicho kinamaanisha kwamba wanahofia kukanusha.



Membe alisema kitabu hicho chenye kurasa 672, kina sura nzima inayozungumzia suala la rada akitaja kwamba, imeandikwa kwenye ukurasa wa 218 na 219.... “Ukienda ukurasa wa 285 utakuta wanaeleza namna fedha zilivyoibwa,” alisema. Hata hivyo, juzi alishindwa kuwataja baada ya Waziri Chikawe kuzima suala hilo.


Kutokana na msimamo wake huko, alijikuta katika shinikizo la kutakiwa kuwataja watuhumiwa hao juzi, wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13.

Wenje kwa upande wake, alisema kambi hiyo inaendelea kuhoji ni kwa nini mpaka sasa watuhumiwa wa kashfa hiyo wanaendelea kutembea vifua mbele bila kuchukuliwa hatua.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alimtaka Membe kuwataja watuhumiwa hao kwa kuwa amesema mara kwa mara kwamba anawajua... “Waziri Membe alipata kueleza anawafahamu watuhumiwa wa kashfa hiyo ni vyema akawataja ili jamii iwatambue.” Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa naye alimtaka Membe kufanya hivyo kwa kuwataja watu waliohusika katika kashfa hiyo.

Kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Silaha ya BAE Systems ya Uingereza, ilianza mwaka 2000 na imekuwa ikiibuka mara kwa mara.
Ilimfanya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Clare Short wakati wa Serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair, kujiuzulu akipinga Uingereza kuuzia nchi maskini kama Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa.

Kashfa hiyo kwa muda mrefu pia imekuwa ikitajwa kumhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge ambaye pia aliwahi kukutwa na kiasi cha Sh1.2 bilioni, kisiwani Jersey ambazo Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ilikuwa ikichunguza kama zilikuwa na uhusiano na biashara hiyo.

Pia kuna kesi ya rada katika Mahakama ya Kisutu huku Polisi ikiendelea kumtafuta aliyekuwa dalali wa biashara hiyo, Sailesh Vithlan ambaye anatuhumiwa kushawishi na kuhonga baadhi ya maofisa wa juu na wanasiasa nchini ili wanunue rada hiyo.

Hata hivyo, tayari Serikali imekwishapokea Pauni 29 milioni za malipo ya fidia kwa Serikali ya Tanzania na imekubaliwa kwamba fedha hizo zitatumika kununua vitabu na madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

No comments:

Post a Comment