Sep 21, 2012


‘Hukumu’ wagombea CCM kuanza leo

KAMATI ya Maadili ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajia kukutana  leo mjini Dodoma kwa ajili ya kupitia mapendekezo yaliyotolewa na vikao vya Sekretarieti kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho.

Kamati hiyo, inakutana siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya Kamati Kuu (CC), ambavyo vinatarajiwa kuanza hapo kesho na kumalizika keshokutwa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, mwanzoni mwa wiki hii aliwaambia waandishi wa habari kuwa vikao hivyo vina lengo la kupitia majina ya wagombea na kutoa mapendekezo yake kabla ya Halmashauri Kuu (NEC) kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea.

Jana Sekretarieti hiyo, ilikuwa ikiendelea na vikao vyake ambavyo vilitarajiwa kumalizika jana.

Hata hivyo,  hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusina na vikoa hivyo, kutokana na maelezo kuwa vikao hivyo ni vya ndani.

Alisema  baada ya Kamati Kuu kumaliza vikao vyake keshokutwa, NEC itakutana kwa ajili ya kuteua wagombea na kumaliza kikao vyake siku inayofuata.

“Kikao cha NEC ndicho kitateua majina ya wagombea na baada ya hapo, ratiba ya uchaguzi itatolewa na baadaye Mkutano Mkuu utakutana mwishoni mwa Novemba kwa ajili ya uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama,” alisema.

Nape alitoa onyo kwa wagombea ambao wanadhani majina yao yatapitishwa kwa kutoa rushwa na kuwataka wagombea kujiepusha na matapeli.

Vikao hivyo, vinatarajia kuchuja majina kuanzia katika jumuiya za chama na nafasi za uenyekiti na makamu mwenyekiti ngazi za wilaya na mikoa.

No comments:

Post a Comment