Sep 10, 2012

YALIYOMO KWENYE MAGAZETI NYUMBANI,,,,

HAPONI MTU

Na Mwandishi wetu, Dar Iringa
TUKIO la kuuawa kikatili, Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, lina mshindo mkubwa na hali halisi ilivyo ni wazi hatapona mtu kutoka kila upande uliohusika.
Habari zinasema kuwa namna tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, inavyotakiwa kufanya kazi, ni lazima itaibuka na majibu yatakayowamaliza wahusika.
Risasi Jumamosi, limenasa taarifa kwamba kuna waandishi wa habari, hususan wale waliokuwepo eneo la tukio siku Mwangosi anauawa, wamekuwa wakipewa msukosuko ili kuwakata kilimilimi wasije wakanena mazito kwenye tume.
Imebainishwa kuwa tayari baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa wanatafutwa mara kwa mara, wameshaondoka Iringa kupisha vuguvugu linaloendelea kwa sasa mkoani humo.
Mwandishi mmoja (jina tunalo) aliliambia Risasi Jumamosi: “Iringa hakukaliki. Kila mara tunapewa vitisho tujitokeze, sijui wanataka kutufanya nini. Sisi tuko makini na kifo cha mwenzetu na tutakapoitwa mbele ya tume, tutaeleza ukweli.”
Wakati tume hiyo ya Nchimbi inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Stephen Ihema ikianza kazi, inaelezwa kwamba itapitia sakata hilo kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
Mmoja wa wajumbe wa tume hiyo aliliambia gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina: “Kuna mambo ya mwanzoni, wakati wa tukio na baada. Maeneo hayo yote tutayaangalia kisha tutakabidhi ripoti ya tume yetu kwa mheshimiwa waziri.
“Tume yetu inafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Hata tulipoteuliwa, hatujapewa muongozo wa kuficha baadhi ya mambo. Tunatakiwa kuchunguza kiini na ukweli halisi. “Umakini wa tume yetu utajionesha baada ya kukabidhi ripoti yetu.”
Alipoulizwa kuhusu kile walichokibaini katika hatua za awali, alijibu: “Huo siyo utendaji mzuri. Sisi ni watu wenye maadili, siwezi kusema tumeona nini hata kama yapo tuliyokwishayaona. Wewe fahamu tu kwamba tupo kazini na majibu ya tume yataonekana kwenye ripoti ya mheshimiwa waziri.”
Pamoja na ugumu wa kupata ‘a-b-c’ za awali ndani ya tume, imeelezwa kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeo (Chadema), hususan Katibu Mkuu, Dk. Willibroad Slaa, wana kazi ya kujieleza mbele ya tume hiyo.
Slaa, atajieleza pia mbele ya tume hiyo kwa sababu kabla ya siku ya tukio, anadaiwa kupishana maneno na Jeshi la Polisi kuhusu amri ya serikali iliyokataza mkusanyiko wa aina yoyote wa vyama vya siasa katika kipindi cha sensa.

Habari zinasema pia kwamba viongozi wa Chadema Mkoa wa Iringa, watahojiwa kwa sababu wao ni sehemu ya chanzo cha mkusanyiko uliosababisha kifo cha Mwangosi wakati polisi walipokuwa wanawatawanya.
Inaelezwa kuwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na askari wake, hasa wale waliotekeleza oparesheni ya kuwatawanya Chadema, Kata ya Nyololo, Mufindi, watahojiwa na tume.
Sababu kuu ni kwamba, Mwangosi alifikwa na mauti akiwa katikati ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kumekuwa na tuhuma nyingi zinazowahusisha polisi na kifo cha mwandishi huyo.
Mwangosi, aliuawa Septemba 2, 2012, Kijiji cha Nyololo, Mufindi Iringa wakati wa vurugu za polisi dhidi ya wafuasi wa Chadema. Katika tukio hilo, afande mmoja ambaye ni jirani na marehemu kwenye makazi alijeruhiwa.
Imeelezwa kuwa, marehemu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, alilipukiwa na kile kinachodaiwa ni bomu wakati akidhibitiwa na maafande wa Jeshi la Polisi.
Habari zinasema kwamba, Mwangosi aliingia kwenye zahama hiyo alipokwenda kuwahoji polisi sababu ya kumkamata mwandishi wa Gazeti la Nipashe, Godfrey Mushi.

No comments:

Post a Comment