Jul 31, 2012

GRAND MALT NA ZFA WATOA POLE KWA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR





Meneja Masoko wa Kinywaji cha Grand Malt, Fimbo Buttalah (kulia) akimkabidhi makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddy hundi ya shilingi milioni tano kama sehemu ya rambirambi zilizotolewa kwa pamoja kati ya Grand Malt ambao ni wadhamini wa Ligi kuu ya Zanzibar na Chama cha Soka Zanzibar ZFA. Kushoto ni Makamu wa rais wa ZFA Kassum Suleiman.
Meneja Masoko wa Kinywaji cha Grand Malt, Fimbo Buttalah (kulia) akimkabidhi makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddy Fedha Shilingi milioni tano kama sehemu ya rambirambi zilizotolewa kwa pamoja kati ya Grand Malt ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu ya Zanzibar na Chama cha Soka Zanzibar ZFA. 
Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddy akizungumza katika hafla fupi ofisini kwake wakati akipokea fedha taslimu shilingi milioni tano toka Grand Malt na ZFA kwa ajili ya kuwafariji wale wote waliopatwa na maafa ya ajali ya meli hivi karibuni.
(Picha zote kwa hisani ya Intellectuals Communications Limited)

WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Zanzibar, ambao ni kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt kwa kushirikiana na chama cha mpira wa miguu Zanzibar (ZFA), wametoa mkono wa pole kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiwa ni kiasi cha Sh milioni 5, kwa ajili ya waathirika wa ajali ya boti ya MV Skagit, iliyotokea hivi karibuni.
Akikabidhi pole hiyo kwa Makamu wa Pili wa SMZ, Balozi Seif Idd, Meneja Masoko wa Grand Malt, Fimbo Butallah alisema wameguswa na tukio hilo na wameamua kuungana na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu.
“Tumeguswa na tukio hili na kama Grand Malt ambao tuko hapa Zanzibar kama wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya hapa, tumeamua kuungana nanyi katika kipindi hiki.
“Tunapenda kuwapa pole wote waliofiwa na wale wote waliokuwemo katika boti hiyo na kwa ujumla kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla,” alisema.
Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam naye alisema walishitushwa baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo na kuamua kuungana na wengine katika kutoa pole yao.
Makamu wa rais wa chama cha mpira wa miguu zanzibar (ZFA) Ally Mohamed, Kassim Suleiman naye alisema walishitushwa pia na ajali hiyo, kwani wamepoteza watu ambao walikuwa mhimili mkubwa katika maendeleo ya mchezo huo visiwani.
Balozi Idd, aliwashukuru Grand Malt kwa pole yao na kusema atafikisha salamu zao kwa wahusika na kuitaka pia iendelee kuwa na moyo huo wa kusaidia pia michezo ndani ya Zanzibar.
Ajali ya MV Skagit ilitokea hivi karibuni katika eneo la Chumbe, Zanzibar na kupoteza maisha ya Watanzania kadhaa.

No comments:

Post a Comment