Aug 8, 2012

UPELELEZI WA KESI YA RAIS WA CHAMA CHA MADAKTARI HAUJAKAMILIKA.

UPELELEZI wa kesi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Namala Mkopi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Mwanaisha Komba, jana alimueleza hayo Hakimu Mkazi, Faisal Kahamba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Kahamba aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, mwaka huu, itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Katika kesi hiyo, Dk. Mkopi anakabiliwa na mashitaka mawili, likiwamo la kutotii amri ya mahakama ya kuzuia mgomo wa madaktari na uhamasishaji wa mgomo huo kinyume cha sheria.

Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, akisaidiana na Wakili Ladslaus Komanya, ulidai kati ya Juni 26 na 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Rais wa MAT, hakutii amri iliyotolewa na Mahakama Kuu Tanzania, Kitengo cha Kazi Juni 26, mwaka huu.

Ilidaiwa kuwa amri hiyo ilimtaka Dk. Mkopi kuwatangazia wanachama wake kwamba wamezuiwa kushiriki katika mgomo kama amri ya awali iliyotolewa na Mahakama hiyo, Juni 22, mwaka huu.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa Juni 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa mjumbe wa MAT aliwashawishi wajumbe wa chama hicho kufanya mgomo kinyume cha amri iliyotolewa na Mahakama Kuu Tanzania, Kitengo cha Kazi, Juni 22, mwaka huu.

Mshitakiwa huyo anatetewa na jopo la mawakili wanne, likiongozwa na Isaya Matamba, Dk. Maulid Kikondo, Dk. Gaston Kennedy na Dk. Rugemeleza Nshala.

Kwa sasa, Dk. Mkopi yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya Sh 500,000.

Wakati huohuo, kesi ya tuhuma za rushwa, inayomkabili Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma (CCM), Omary Badwel, imeahirishwa kwa sababu mbunge huyo amefiwa na dada yake.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Lizzy Kiwia, alidai kwa Hakimu Mkazi Faisal Kahamba kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na wana shahidi mmoja, lakini mshitakiwa amefiwa na dada yake.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Kahamba aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, mwaka huu, itakapoanza kusikilizwa.

Badwel katika kesi hiyo namba 146 ya mwaka 2012, anakabiliwa na mashitaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa na anatetewa na Wakili Mpale Mpoki.

Katika hatua hiyo ya awali, mshitakiwa alisomewa maelezo ya mashitaka na kupewa nafasi ya kubainisha mambo au maelezo anayoyakubali na asiyoyakubali ambayo upande wa mashitaka utapaswa kuleta ushahidi mahakamani kuyathibitisha.

Badwel anadaiwa kukamatwa na TAKUKURU akipokea rushwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana, katika Hoteli ya Peacock ya Dar es Salaam, baada ya kumwekea mtego.

No comments:

Post a Comment