Bunge lakubali kwa kauli moja
*Muswada kuwasilishwa Oktoba
*Spika Makinda aitwisha kazi wizara
*Hoja ya Jaffo yawakuna wabungeWABUNGE wamekubali kuwasilishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria Hifadhi ya Jamii, kwa hati ya dharula katika mkutano wa Bunge lijalo.
Muswada huo, utawasilishwa baada ya Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM) kutoa maelezo binafsi kutaka mswada huo uletwe Bungeni ili uweze kufanyiwa marekebisho.
Kufuatia maelezo hayo na hoja hiyo kuungwa mkono na wabunge, Spika wa Bunge Anna Makinda aliiagiza Wizara ya Kazi na Ajira kupitia maelezo ya Jafo na kupelekaa Muswada huo katika Bunge la Tisa.
“Kwa kuwa hoja hii imeungwa mkono, kesho (leo) Wizara ya Kazi na Ajira, itapitia maelezo ya mheshimiwa Mbunge na katika Bunge la Tisa Muswada, utaletwa kwa njia ya dharula kutokana na umuhimu wa jambo hilo,” alisema Spika.
Akitoa maelezo yake, Jafo alitaka Muswada huo, upelekwe bungeni ili kuweka kifungu ambacho kinaruhusu kuwepo kwa fao la kujitoa.
“Kabla ya Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufanyika kupitia Sheria ya Marekebkisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, namba 5 ya mwaka 2012, kulikuwepo na utaratibu wa wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufaidika na fao la kujitoa.
“Utaratibu huu, uliwawerzesha watumishi walioacha au kuachiwa kazi kabla ya kutimiza umri wa kustaafu miaka 55 au 60 kulipwa mafao yao ya uzeeni, na hivyo kupata kianzio cha kuendesha maisha yao baada ya kuacha kazi.
“Utaratibu huu, pia uliwezesha hata watumishi ambao walikuwa bado wapo kazini, kutumia kiasi cha mafao yao ya uzeeni kwa ajili ya kuwawezesha kujijengea nyumba na pia kupata mitaji au kianzio cha kufanya shughuli nyingine za kuwapatia kipato cha kuanza kujiwekea mazingira mazuri na kufanya maandalizi ya maisha ya kustaafu.
“Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Jamii namba 5 ya mwaka 2012, haikuweka kifungu chochote cha Sheria kwa ajili ya kuweka misingi ya kisheria kuwezesha kuwepo kwa fao la kujitoa.
“Kutokuwepo kwa vifungu vya sheria vya kuwezesha kuwepo kwa fao hilo, kutaleta athari kubwa kwa watumishi ambao wataacha kazi au kuachishwa kazi kabla ya kufikisha umri wa kustaafu na hivyo kuhitaji fedha za kuendeshea maisha yao.
“Jambo hili, limekuwa tete katika maeneo ya nchi kiasi cha kushusha uzalishaji hasa katika sekta ya madini na hiyo imejidhihirisha wazi kwa wafanyakazi wa migodi ya madini kuitisha migomo na kufanya maaandamano,” alisema.
Alisema sababu za wafanyakazi kupinga kuondolewa kwa fao hilo ni kuwa wafanyakazi wengi hawana uhakika wa kutumikia sekta hizo mpaka watimize miaka 55 hadi 60, hivyo kutokuwepo kwa fao la kujitoa ni kuwanyima haki zao.
“Mheshimiwa Spika, kunapotokea tatizo linalogusa sehemu kubwa ya Jamii, Bunge lako tukufu lina wajibu wa kulisema kwa kuitaka Serikali itafute ufumbuzi wa haraka.
“Kwa sababu hiyo, naomba niwasilishe maelezo binafsi, ushauri na maelekezo kwa Serikali ili ilipatie ufumbuzi wa haraka suala hili.,” alisema
Alisema kuna kila sababu na umuhimu kwa Serikali kupeleka Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mfuko wa Jamii, kwa ajili ya kuweka vifungu vya Sheria vinavyoruhusu fao la kujitoa.
“Muswada huo, pia uweke vifungu vya sheria vinavyoruhusu watumishi kutumia kiasi cha mafao ya uzeeni kwa ajili ya kulipia au kugharamia shughili nyingine yeyote ili kujiwekea mazingira na pia kujiandaa na kustaafu.
“Katika Muswada huu, Serikali iondoe vifungu katika sheria hiyo, vinavyoweka masharti ya kumtaka mtumishi kuwasilisha maombi kwa Rais, kupitia utaratibu wenye urasimu mkubwa ya kupewa msamaha wa kutobanwa na masharti yanayozuia fao la kujitoa au kutumia kiasi cha mafao ya uzeeni pale anapohitaji kuliapwa mafao ya kujitoa kwa ajili ya kuendesha maisha yake.
“Serikali iyaagize makampuni ya madini hususan mgodi wa Bulynhulu, kutomsimamisha mfanyakazi yeyote aliyehoji kwa kina juu ya mafao yao baada ya kupatwa na mshtuko wa taarifa ya kutoruhusiwa kuchukua mafao yao baada ya kuacha au kuachishwa kazi.
“Wakati tunasubiri kuletewa Muswada huo kwa hati ya dharula, Serikali itoe Waraka maalum wa maelekezo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuendelea kuwalipa mafao yao ya watumishi walioacha kazi au kuachishwa kazi, kabla ya kufikisha umri wa kustaafu.
“Katika Muswada huo, Serikali iangalie upya Kanuni inayotumika katika ukokotoaji wa mafao kwa watumishi waliostaafu ili kutozua balaa linguine kwa siku za usoni.
“Aidha, Serikali iangalie uwezekano wa kuweka utaratibu wa watumishi wote wanaolipa kodi kupitia mishahara yao kupewa TIN Namba ili watambulike kama ni walipa kodi halali ndani ya nchi yetu kuliko inavyoendelea hivi sasa.
No comments:
Post a Comment