Aug 6, 2012

URAISI WAMTESA ZITTO KABWE.

JINAMIZI la urais linaendelea kumwandama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA).


Asema hajawahi kutangaza mwaka
*Akiri ni vigumu bila baraka za chama
*Aahidi kumuunga mkono atakayeteuliwa
*Masha naye aibuka, autolea macho ubunge


Hali hiyo imetokana na mwanasiasa huyo machachari kushindwa kuweka wazi mwaka wa uchaguzi ambao atagombea urais kama ambavyo amekwisha kutangaza.

Zitto alipatwa na kigugumizi hicho jana alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Makutano kinachorushwa na radio ya Magic FM ya Dar es Salaam.

Zitto alihojiwa kuhusu masuala mbalimbali na katika suala la urais aliendelea kusisitiza kuwa anautaka ingawa alishindwa kutaja mwaka ambao atatekeleza azma yake.

Zitto alisema suala la kugombea urais ni azma yake kutoka moyoni na kueleza kuwa yeye ni tofauti na wanasiasa wengine ambao hulitaka jambo kwa kisingizio cha kutumwa na watu wengine.

“Ni kweli nautaka urais jambo ambalo nataka Watanzania wajue, mimi sikusema ni lini lakini nia yangu ipo…iwe mwaka 2015, 2020 au 2025.

“Dhamira yangu nataka siku moja kuliongoza taifa langu, kama mwanasiasa mkomavu huu ni uamuzi wangu kutoka moyoni, sijatumwa wala kuagizwa na mtu yeyote.

“Siamini katika kauli za kutumwa, kuombwa wala kuagizwa ila kwa mwanasiasa anayejiamini katika uongozi lazima athubutu kuweka dhamira ya kweli katika kuongoza wananchi,”alisema Zitto.

Hata hivyo, Zitto alisema pamoja na dhamira yake hiyo, ataendelea kufuata sheria na taratibu ambazo ni pamoja na kupata ridhaa ya chama chake cha CHADEMA.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema hadi hivi sasa chama chake hakina mgombea urais na kueleza kuwa muda ukifika suala hilo litakuwa bayana.

Zitto alisisitiza kuwa hana ubinafsi juu ya hoja hiyo na kusema kuwa mwanachama yeyote atakayeteuliwa kupeperusha bendera katika wadhifa huo yuko tayari kumuunga mkono.

Akizungumzia suala la tuhuma za rushwa linalohusisha wabunge kuhongwa na kampuni na baadhi ya makampuni ya mafuta, Zitto alirejea msimamo wake wa kupinga kuhusika katika rushwa.

Zitto alisema binafsi yake anaiamini tume iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda katika kushughulikia sakata hilo kwa kusema kuwa ripoti ya tume hiyo itabainisha ukweli iwapo anahusika au laa.

“Kwa sasa tumekuwa katika taifa la majungu, uwongo, fitna na tuhuma zisizokuwa na maana na haya yamekuwa kama maisha ya kawaida ya wananchi.

“Nadhani kwa hili tusiliongelee sana na tuiachie tume iliyoundwa kuchunguza jambo hili ifanye kazi kwa uhuru mkubwa..kwani inatakiwa kutoa majibu yake ndani ya siku 14…msihofu majibu yatatoka tu hivu karibuni,”alisema Zitto.

Zitto pia alisisitiza kuwa yeye siyo mla rushwa na wala hajawahi kula rushwa.

Mwanasiasa huyo kijana anadaiwa kuwa na utajiri mkubwa na baadhi ya mali anazodaiwa kuwa nazo ni pamoja na ujenzi wa kasri unaoendelea Mbezi Dar es Salaam na magari ya kifahari.

Katika mahojiano hayo, Zitto alikanusha madai hayo akisema maneno yote hayo yaliyoibuka ni fikra hasi juu ya nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

“Dhamana niliyonayo katika POAC inawajenge watu sura tofauti ya labda najinufaisha na madaraka yangu katika kamati hiyo…nasimamia mashirika zaidi ya 290, kwa hiyo wanafikiri Zitto ni tajiri.

“Na kama vile haitoshi ule msimamo wangu kupinga posho za ubunge nayo ilifanya wengi wachukie …lakini nitaendelea na msimamo wangu ule ule.

“Kuhusina na mali zangu ..mimi si tajiri kama wengi wanavyodhani, sina Range Rover, Hammer au jumba la fahari kama watu wanavyozusha.

“Mimi ninajenga Kigoma, Dar es Salaam sina nyumba, sina kiwanja achilia mbali kiwanja sijawahi kuomba kiwanja Dar es Salaam wala Dodoma, hilo kasri nitakuwanalo wapi?.

“Nakumbuka siku hiyo mambo haya yaliibuka ilikuwa siku ambayo bajeti ya Nishati na Madini ilikuwa inawasilishwa ….na katika wakati mwengine siku hiyo hiyo, mishahara na posho mpya kwa wabunge zilianza kutoka, hivyo basi wabunge wengi walichangia jambo hilo hadi wengine wasiopenda kuzungumuza siku hiyo walizungumza,” alisema Zitto.

Alipohojiwa juu ya kiasi kipya cha posho na mshahara Zitto alikataa katu katu kuzungumzia hoja hiyo na kusema kuwa mtu wa kuulizwa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Wakati huohuo, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha alisema bado anayo dhamira ya kuwania tena ubunge katika jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza.

Masha aliangushwa na mbunge wa sasa jimbo hilo, Ezekia Wenje wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010 na hivyo kupoteza ubunge pamoja na uwaziri.

Masha ambaye alikuwa akihojiwa katika kipindi hicho alisema bado anayo dhamira ya kugombea tena kiti hicho cha ubunge wa Nyamagana lakini hajaamua atafanya hivyo lini.

Alisema kuwa hawezi kutangaza ni lini atafanya hivyo lakini iwapo wananchi wa jimbo hilo watamuhitaji kugombea uchaguzi ujao wa 2015 atafanya hivyo.

“Nikigombea tena sitashindwa …suala la kutaka kugombea ni lazima lakini kwa sasa nafanya biashara zangu binafsi…najipanga nitarudi tena katika siasa,” alisema Masha.

No comments:

Post a Comment