Aug 6, 2012

MSIMAMO MKALI WA MAKAMBA KWA CCM

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, ameweka hadharani msimamo wake kuhusu mwenendo wa chama chake.

Katika msimamo huo, Makamba amesema kuwa yeye ni mwachama mwaminifu kwamba hana ndoto za kukihama chama hicho hata kama kitachafuka vibaya.

Makamba amepuuza kelele za wapinzani wanaodai kuwa kifo cha CCM kipo jirani na kueleza kuwa ataendelea kukitumikia chama hicho hadi kifo chake.

Makamba alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Shirika la Maendeleo la Bumbuli (BDC) ambalo limelenga kuinua uchumi wa wananchi wa jimbo hilo.

Makamba alikuwa akifanya mazungumzo na Mtanzania Jumapili muda mfupi kabla ya kuingia katika mkutano wa Shirika la Maendeleo la watu wa Bumbuli (BDC) uliofanyika jana Karimjee, Dar es Salaam.

Makamba alisema amekuwa katika chama hicho tangu ujana wake na hivyo ataendelea kukitumikia hadi mauti yatakapomfika.

“Nilikuwa humu humu na nitaendelea kuwa humu humu mpaka kifo changu hata kama chama kinafanya vibaya….nimetoka mbali sana na chama hiki,” alisema.

Makamba alisema alipokuwa shule alipendelea kufanya kazi katika Shirika la Posta, lakini bahati mbaya aliteuliwa kusomea ualimu ambapo alifundisha kwa miaka nine kabla ya kujiunga na CCM.

“Nimepita na chama hiki kwenye milima na mabonde na haitatokea hata siku moja kwenda tofauti na chama changu…narudia nilikuwa humu na nitaendelea kuwa humu humu mpaka kufa,” alisema mzee Makamba.

Makamba pia aliwataka wananchi kuwa na moyo wa kujituma katika kufanya kazi na kueleza kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hawezi kupatikana kwa kujibweteka.

Alisema hakuna kiongozi au chama chohote cha siasa ambacho kitawaletea maenendeleo wananchi ambao hawajishughulishi.

“Imeandikwa katika vitabu vitakatifu vya mungu fanyeni kazi ili mpate mkate wa siku…sasa kama vitabu vya Mwenyezi Mungu vimeandika wewe itakuaje ushindwe kujituma?” alihoji Makamba.

Alikwenda mbali zaidi na kuwataka wazazi wasiwaandae watoto wao kuwa watumishi wa ndani (mayaya) na badala yake wawape fursa ya kujisomea kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

“Nashangaa sana wazazi wa kitanzania …huku wanalalamika maisha bora na wakati hata maisha ya watoto ya baadaye ya watoto wao wanayaharibu wenyewe.

“Wazazi hawa hawa wamewageuza watoto wao yaya….mtoto anatoka shuleni anafikia kulea mdogo wake, kweli huyu mtoto atasoma kwa ufanisi?

“Mfano si mnawaona vijana wangu hawa…sasa kama mimi na mama yao tungewafanya yaya kweli wangefika hapa walipo?” alihoji mzee Makamba na kuwahimiza wazazi wa kitanzania kusimamia elimu ya watoto wao.

Kwa upande wake Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Bumbu (BDC), alisema Shirika lake limelenga kuinua uchumi wa wananchi wa jimbo lake.

January ambaye pia Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alisema shirika lake litakuwa la kimataifa ambapo litakuwa na wakurugenzi 12.

No comments:

Post a Comment