Jul 27, 2012

BUNGENI LEO....

Wabunge wadaiwa kufanya kampeni chafu..
WAKATI wabunge wakikiri kukosa umakini katika utungaji wa sheria, baadhi yao wamedaiwa kuanza kampeni chafu kutetea kampuni inayotia hasara ya Sh bilioni 6 kwa serikali kwa mwezi, ili ipewe zabuni iendelee kufyeka fedha za walipakodi kupitia Shirika la Umeme (Tanesco).  Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) jana alidai kuwa Bunge limeonesha dalili ya kukosa umakini kwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Aprili mwaka huu ambayo mwaka haujapita, wanaomba kuijadili baada ya kulalamikiwa na wafanyakazi. Mbunge wa Kuteuliwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akiongozana na wabunge wa chama hicho jana, aliitisha kikao na waandishi wa habari na kudai kuwa baadhi ya wabunge hao hivi sasa wanafanya kampeni ndani na nje ya Bunge kutetea kampuni hiyo inayochota fedha. Kwa mujibu wa madai ya Mbatia, wabunge hao aliowafananisha na majambazi, wanafanya kampeni ili makadirio ya Bajeti ya Nishati na Madini yatakapofikishwa bungeni leo, waungwe mkono kutetea kampuni hiyo iendelee kutia hasara serikalini. Mbatia alidai kampuni hiyo kwa kufuata Sheria ya Manunuzi, ilishinda zabuni ya kuiuzia Tanesco mafuta mazito kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kwa Sh 1,800 kwa lita. Hata hivyo, pamoja na kushinda zabuni iliyopitishwa na
Bodi ya Zabuni ya Tanesco, mnunuzi wa mafuta hayo si Tanesco, ni Serikali. Kutokana na hali hiyo, Mbatia alidai kuwa, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ambaye ndiye mtoa fedha, alikataa kuipa fedha kampuni hiyo na kuipa kampuni ya Puma Energy Tanzania Ltd ambayo ilishindwa katika mchakato huo wa zabuni. Kwa mujibu wa madai ya Mbatia, Maswi alitoa fedha kwa kampuni ya Puma kwa sababu mbili; mosi bei yake ya mafuta kwa Tanesco ni ndogo sawa na Sh 1,460 kwa lita tofauti na kampuni inayodaiwa kutetewa na wabunge ambayo ingeuza mafuta hayo kwa Sh 1,800 kwa lita. Kwa hesabu hizo, Mbatia alidai kuwa uamuzi wa Maswi umeokoa Sh bilioni 6 za Serikali kwa mwezi ambazo kama kampuni inayodaiwa kutetewa na wabunge ingelipwa, zingepotea. Sababu ya pili ya Maswi kuipa kampuni hiyo kazi ya kuiuzia Tanesco mafuta kwa mujibu wa madai ya Mbatia, ni kwa kuwa asilimia 50 ya hisa za kampuni ya Puma zinamilikiwa na Serikali na hivyo faida yake kuwa sehemu ya mapato ya Serikali. Mbatia alidai wabunge hao wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wanawashawishi wabunge waitetee kampuni hiyo kwa kutumia hoja ya kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi na kupuuzia hoja ya kuepusha upotevu wa fedha za walipa kodi Sh bilioni 6 kwa mwezi. Alidai baadhi ya wabunge hao ni wajumbe wa Bodi ya Tanesco, jambo alilodai kuwa hatua yao ya kuwashawishi wabunge wengine wawaunge mkono, inawafanya waamini huenda wamepata kitu kwa kuwa inaleta mgongano wa maslahi. Alidai wabunge hao wanataka kuwajibisha uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa mbali na kuinyima kampuni hiyo fedha, pia imehoji fedha za Tanesco zinapokwenda. Mbatia alidai kuwa Tanesco kuna matumizi mabaya ya fedha kwa kuwa baada ya kupandisha bei ya umeme Januari mwaka huu, kwa mwezi imekuwa ikipata wastani wa Sh bilioni 60. Kwa mujibu wa madai ya Mbatia, Mei mwaka huu shirika hilo lilikusanya Sh bilioni 85 wakati matumizi yake kwa mwezi ni Sh bilioni 11 na kuhoji fedha zingine zinapopelekwa wakati shirika hilo halinunui mafuta. Maswi akizungumza na blog, alisema kuna siasa nyingi katika suala hilo na asingependa kulizungumzia. Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Selemani Jumanne Zedi hakupatikana kwa simu baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge jana saa 12 jioni. Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Diana Chilolo simu yake iliita bila majibu.

No comments:

Post a Comment