Jul 5, 2012

HASHEEM THABEET ALAMBA BINGO OKC...

Habari ambazo zimetambaa, zinasema kwamba mtanzania anayecheza katika ligi ya kikapu nchini Marekani,(NBA) Hasheem Thabeet, atajiunga na timu ya Oklahoma City Thunders kwa mkataba wa miaka miwili. Kwa mujibu wa Oklahoman, Ingawa mkataba kamili haujawekwa wazi inasemekana kwamba Hasheem ataingia kwa mkataba wa kulipwa mshahara usiopungua $880,000 katika mwaka wa kwanza wa mkataba huo. Oklahoma City Thunders au OKC kama wanavyofahamika miongoni mwa mashabiki wa mpira wa kikapu na ligi ya NBA, itakuwa ni timu ya nne kwa Hasheem Thabeet kuichezea tangu aliposaini na Memphis Grizzlies kufuatia kuwa wa pili katika NBA Draft mwaka 2009 mbele kwa nafasi moja kutoka kwa mchezaji mwingine anayechezea Thunder hivi sasa,James Harden. Hata hivyo,Hasheem ameonekana kutokuwa na mwanzo mzuri sana ndani ya NBA tofauti na alipokuwa chuoni Connecticut ambapo aliwahi kuwa Defensive Player Of The Year. Katika michezo 135 ndani ya NBA, Hasheem ana kiwango cha point 2.2, rebound 2.7 na 0.9 blocked shots. Kwa muda mrefu OKC walikuwa wakimtaka Hasheem na walisikitika mwaka 2009 alipochukuliwa na Memphis. Ni mwanzo mwingine kwa Hasheem Thabeet na kwa jinsi OKC walivyo,basi huenda tukashuhudia msimu tofauti kabisa wa NBA na bila shaka msimu tofauti kwa Hasheem Thabeet.

No comments:

Post a Comment