Jul 25, 2012

KIMATAIFA LEO...

RAISI WA GHANA JOHN ATTA MILLS, AFARIKI DUNIA.
RAIS wa Ghana, Evans John Atta Mills (68) amefariki Dunia katika hosipitali moja ya kijeshi iliyopo mji mkuu wa nchi hiyo, Accra. Mills amekutwa na mauti siku chache tangu aliporejea kutoka Marekani ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Taarifa za mashirika ya habari ya kimataifa zilizotolewa jana jioni zilisema Rais huyo wa tatu wa Ghana aliugua ghafla juzi Jumatatu na alifariki jana mchana baada ya kuzidiwa. Shirika la Uingereza Reuters lilimnukuu mmoja wa wasadizi wa Rais Mills akisema kuwa rais huyo alikuwa amethibitika kufariki jana mchana. Habari zaidi zilisema kwa mujibu wa Katiba ya Ghana, Makamu wa Rais John Dramani Mahama alikuwa akitarajiwa kuapishwa jana usiku kuchukua nafasi ya Mills ili kuongoza taratibu za mazishi ya mtangulizi wake. Katika siku za karibuni afya ya kiongozi huyo imekuwa ikiripotiwa kuzorota na mwaka huu pekee ameshakwenda Marekani mara tatu kwa ajili ya tiba. Mara ya mwisho alionekana hadharani nchini Ghana Juni 3 mwaka huu wakati alipokwenda kutemebelea eneo la ajali ya ndege, ziara ambayo ilizua minong’ono kutokana na wanachi kudai kuwa hakuonekana kuwa mwenye siha njema. Profesa John Evans Fiifi Atta Mills alizaliwa Julai 21, 1944 na aliapishwa kuwa Rais wa Ghana Januari 7, 2009 baada ya kuwa ameshinda uchaguzi dhidi ya mgombea wa kilichokuwa chama tawala Nana Akufo-Addo katika uchaguzi wa 2008.

No comments:

Post a Comment