Jul 13, 2012

KWANINI AKICHELEWA KUPOKEA SIMU UWAZE ANAKU CHEAT???

TUMEKUTANA kwenye kona yetu kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku katika kukumbushana tumekwama wapi na tunapoelekea. Leo ndugu zangu kuna jambo moja nataka tuzungumze kwa pamoja ambalo limekuwa tatizo miongoni mwetu. Nimekuwa nikirudia mara nyingi kuielezea simu katika uhusiano kutokana na watu kuitumia vibaya na kuamini simu ni kipimo sahihi cha uaminifu. Wapo ambao wakirudi nyumbani, lazima wapekue simu za wapenzi wao wajue nani kapiga, kampigia nani na ujumbe ulioingia. Watu wa aina hiyo wakipiga simu na ikachelewa kupokewa au isipokewe kabisa, huumia na kuamini wameshasalitiwa, hujiuliza kama haijapokewa, lazima mpenzi atakuwa anavunja amri ya sita. Matatizo haya japo si kwa kiasi kikubwa hata mimi yaliishawahi kunitokea, lakini baada ya kujifunza, niligundua hili ni janga la wengi. Hii inatokana na watu wengi kushindwa kujua nini maana ya matumizi ya kifaa hicho. Ulimbukeni wa matumizi umekuwa ndiyo njia ya watu kutoka nje ya ndoa au uhusiano wao. Simu imesababisha watu kuwekeana masharti ya kutogusa simu zao. Mada hii niliishawahi kuiandika pale nilipouliza simu na mwili kipi chenye thamani? Kama unaweza kumuachia mwenza wako mwili wako auchezee anavyotaka, kwa nini usimruhusu aishike simu yako? Mada yangu leo nitaielekeza katika matumizi ya kawaida, siyo yale ya kufichiana simu au mtu kwenda kuoga nayo. Kumekuwa na fikira mbaya pale unapompigia mpenzi wako halafu iite kwa muda mrefu bila kupokelewa, lazima wasiwasi utakuingia moyoni mwako, labda umesalitiwa, uongo kweli? Hii imesababisha kuweka migongano katika uhusiano kati ya mtu na mtu. Hata mpenzi wako akijitetea vipi sababu iliyosababisha yeye kuchelewa kupokea, huwezi kukubali, lazima utajua alikuwa na mtu mwingine aliyesababisha asiipokee. Swali linakuja; mpenzi wako akichelewa kupokea hana kingine cha kufanya zaidi ya kukusaliti? Asilimia kubwa ya watu wenye mawazo hayo, ndiyo wenye kuyatenda haya ya upande wa pili. Huwezi kuuogopa unyasi bila kuumwa na nyoka. Mazoea ya simu: Tatizo hili lipo sana kwa wanawake ambao ni wazembe kuwa na simu karibu hasa wanapokuwa nyumbani. Wengi wao wanafikia hatua ya kuwasindikiza mashoga zao na kuiacha simu ndani. Kwa nini uwaze hivyo? Pamoja na baadhi ya watu kukosa uaminifu katika mapenzi, wapo ambao hawapendi kuwa na simu muda wote, anapoiweka hawezi kuibeba mpaka asikie inaita au ambao wanapokuwa kwenye watu wengi kama kituo cha basi au sokoni, huizima kwa ajili ya kuogopa vibaka. Inawezekana unapompigia anakuwa yupo nje na hana mawazo kama ameiacha ndani, akikupigia baadaye bado hutamuamini. Wakati mwingine umempigia simu ikawa haipatikani, akikueleza utamuona mwongo na utadhani alizima kwa sababu alikuwa na mambo yake. Kabla teknolojia ya mtandao haijaingia nchini, watu wengi waliwaamini wapenzi wao. Mpenzi wako kuwahi kupokea simu siyo ishara ya uaminifu, kuna ambaye anaweza kupokea na kukupa maneno matamu ya mapenzi, kumbe yupo juu ya kifua cha mtu. Simu itumiwe kama mawasiliano na wala si kigezo cha kutambua uaminifu wa mwenzako, pia mtu anayechelewa kupokea hana kingine cha kufanya zaidi ya kufanya usaliti? Tubadilike.

No comments:

Post a Comment