Aug 1, 2012

PAPAA MSOFE MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI


Papaa Msofe.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni Jijini Dar es Salaam linamshilikia mfanyabishara maarufu,  Marijan Abubakari maarufu kama Papaa Msofe kwa tuhuma za mauaji. Habari zinasema kuwa Papaa Msofe alikamatwa na Polisi juzi jijini Dar es Salaam na anashikiliwa katika kituo cha Polisi cha Magomeni jijini humo.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha Papaa Msofe kushikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji.
“Ni kweli tunamshikilia Papaa Msofe katika Kituo cha Polisi cha Magomeni na tunaendelea kumhoji na kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio analotuhumiwa nalo,” alisema Kamanda Kenyela.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kenyela, alisema Papaa Msofe alikamatwa baada ya kutokea mauaji ya Onesphori Kituli, mkazi wa Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam.
Alisema kabla ya kutokea mauaji hayo, Papaa Msofe na marehemu walikuwa wakigombea nyumba ambayo ilikuwa imewekwa rehani kwa Sh. milioni 30.
Habari zaidi kuhusiana na tukio hilo ambazo hata hivyo hazikuthibitishwa na Kamanda Kenyela, zinasema kuwa bado kuna mtu mwingine ambaye anahusishwa na tuhuma hizo za mauaji, lakini mpaka sasa hajakamatwa.
Kamanda Kenyela alifafanua kwamba Papaa Msofe alimpa marehemu fedha hizo kwa makubaliano kwamba ikiwa atashindwa kuzilipa atachukua nyumba yake.
Kabla ya mauji hayo ilidaiwa kwamba, Papaa Msofe na mwenzake walikuwa wakimtishia maisha marehemu huyo.
Kamanda Kenyela alisema kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo, marehemu alifungua kesi mahakamani na kwamba siku ya hukumu alikutwa amekufa mbele ya mlango wa nyumba yake na kwamba hakuna mali yoyote iliyochukuliwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya upepelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment