Sep 6, 2012

Nape: Aitaka CHADEMA iwajibike na Mauaji.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwajibika kutokana na kuwepo kwa matukio ya watu kupoteza maisha yanayosababishwa na maandamano ambayo yamekuwa yakifanywa na wafuasi wake.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Chadema wana kila sababu ya kuwajibika, kwa sababu matukio haya ya mauaji yamekuwa yakitokea kwenye operesheni za mikutano yao na matukio ya aina hii kutokea katika kazi za chama cha siasa ni aibu, hivyo viongozi wa kisiasa wanaokutwa na matukio hayo ni lazima wawajibike kwa umma, lakini matukio haya yamekuwa yakitokea bila wao kuwajibika,” alisema Nape na kuongeza:
“Inapotokea shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake.”
Alisema CCM inaungana na wanaCCM na wananchi wote kulaani mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu.
“Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao. CCM inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine,” alisema Nape.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi alisema CCM imetoa mwito kwa vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza kwa umakini na weledi mauaji ya Mwangosi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo pamoja na chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha mwandishi huyo wa habari.


“Pamoja na mwito wetu wa kuchunguzwa suala hili kwa umakini na weledi mkubwa, pia tunatoa rai kwamba uchunguzi huu ufanyike kwa kutumia muda mfupi ili ukweli uweze kubainika mapema na hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema Nape na kuongeza:
“Vilevile CCM inasikitishwa sana na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na Chadema nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na usalama.”
Aliyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni la kuuawa kwa kada wa CCM mkoani Singida, kuuawa kwa Ali Hassan mjini Morogoro, kuuawa kwa Mwangosi, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine yalitokea wakati viongozi wa Chadema wakiendesha operesheni zao mbalimbali nchini.
Nape alisema matukio hayo si mazuri kutokea kwenye shughuli za chama cha siasa kwa madai ni aibu kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla na hivyo kupoteza sifa ya kuitwa chama chema cha siasa.

No comments:

Post a Comment