Sep 4, 2012







RAIS Jakaya Kikwete juzi alikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliouaga mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi na kumwelezea kuwa alikuwa mtu mkweli ambaye hakusita kueleza jambo aliloliamini.
Zenawi aliyefariki Agosti 20, mwaka huu na alitarajiwa kuzikwa jana jijini Addis Ababa.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilisema Rais Kikwete aliwasili Addis Ababa juzi akifuatana  Waziri Mkuu Mstaafu na Katibu Mkuu zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim.
Kikwete alisema, “Zenawi alikuwa mkweli ambaye katika maisha yake hakusita kusema jambo aliloliamini.”
Alisema Zenawi alikuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa kiutendaji na kwamba ameacha pengo kubwa kwa watu wa Ethiopia.
Kikwete aliaga mwili huo uliowekwa kwenye kasri ya Waziri Mkuu, baada ya kutia saini kwenye kitabu cha maombolezo.
Pia Rais Kikwete aliweka shada la maua kwenye jeneza la mwili wa Zenawi na baadaye kuipa pole familia yake akiwemo mjane wa Marehemu Azeb Mesfin, Mbunge  ambaye alipigana vita vya msituni akiwa na Zenawi.
Mbali na Dk Salim, ujumbe wa Tanzania kwenye mazishi hayo uliwasilishwa na Mabalozi wa Zamani wa Tanzania nchini Ethiopia, Jenerali Sam Hagai Mirisho Sarakikya na Christopher Liundi.
Wengine ni  Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Haroub Ali Suleiman na wabunge Livingstone Lusinde (Mtera) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini).

No comments:

Post a Comment