Sep 4, 2012

YOU MUST READ THIS...


CCM yawakaanga Bashe, Kigwangalla

SAKATA la makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangalla kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya uongozi wa chama hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili walishughulikie kimyakimya ndani ya chama kwa madai kuwa linakifedhehesha chama.
Tayari taarifa zimeeleza kuwa chama hicho jana kiliwaandikia barua ya kuwaita kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya makada hao kuwataka wajieleze kwa tukio la kugombana hadharani.
Katibu wa CCM Mkoa Tabora, Idd Ame alithibitisha kutoa agizo kwa uongozi wa chama hicho Nzega kushughulikia suala hilo nje ya dola na kueleza kuwa kinachofanyika sasa ni utekelezaji wake.
“Tulikwisha kutoa maelekezo kwa Katibu wa CCM wa Wilaya wa namna ya kushughulikia suala hili. Atakuwa anajua zaidi mkimuuliza,” alisema Ame.


Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyohoroka alisema kuwa makada hao wataitwa kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa kwa agizo la CCM mkoa.
Baada ya kikao hicho, mapendekezo yake yatapelekwa kwa Katibu wa mkoa ambaye ndiye aliyeagiza kifanyike,” alisema Vyohoroka.
Hata hivyo, Vyohoroka alisema kuwa kwa itifaki ya CCM, yeye hataueleza umma mapendekezo ya kikao hicho, badala yake atakayefanya hivyo ni Katibu wa CCM wa Mkoa. Hatua hiyo ya CCM kutaka kushughulikia suala hilo nje ya mkono wa dola limekuja huku polisi ikiwa bado inaendelea na uchunguzi wake.

Dk Kigwangalla akataa suluhu
Dk Kigwangalla alithibitisha kupokea barua ya kuitwa katika kikao hicho na kusema kwamba anatambua kuwa ni cha dharura mahsusi kwa ajili ya kuwasuluhisha. Hata hivyo, alisema hayupo tayari kukubaliana na jambo hilo.
“Nimepokea, barua ya wito wa kikao najua wanataka kutusuluhisha, lakini nasema sipo tayari kwa sababu chama wanataka kusuluhisha suala hili wakati mimi nimeshachafuka, sitakubali,” alisema.
Awali, Dk Kigwangalla alisema alifikiria kuachana na suala hilo kwa kuwasamehe wote waliomkosea isipokuwa Bashe lakini sasa amebadili mawazo.
“Nilianza kufikiria kuwasamehe walau wale walionishambulia kwa matusi na kunisukuma kwa dharau. Nilitaka abaki yule aliyetishia kunipiga risasi na kuniwinda, lakini sasa siko tayari kufanya hivyo, nitaendelea na kesi hii hadi mahakamani na ukweli utadhihirika kule na haki itatolewa,” alisema.
Alisema uamuzi wake umekuja kutokana na kuona ameanza kugeuziwa kibao huku akisema imani yake ni kuwa atapiganiwa na Mungu.
Bashe ataka mkondo wa sheria
Bashe alisema hajapata barua ya kuitwa kwenye kikao hicho ila anayo taarifa kwamba kikao hicho kinafanya tathmini ya uchaguzi uliofanyika wilayani humo.
“Sina barua na sasa niko safarini kuelekea Dar es Salaam. Ninachojua kikao hicho ni cha tathmini ya uchaguzi na Kigwangalla ameitwa kwa kuwa ni mjumbe. Mimi siyo mjumbe, lakini kama watajadili suala hilo wanaweza kuniita,” alisema
Hata hivyo, alieleza kuwa msimamo wake ni kutaka suala hilo liende mahakamani ili kulinda heshima ya chama hicho.
“Niseme tu kwa kifupi kwamba, utaratibu wa sheria unapaswa kuheshimika.”
Alisema ili chama kiheshimike kinapaswa kusimama kwenye sheria hivyo haoni sababu za uamuzi wa suala hilo kuondolewa polisi kwa vile ndicho chombo husika kwa masuala hayo.RPC asisitiza uchunguzi
Kamanda wa Polisi Mkoani wa Tabora, Antony Lutta alisema kwa simu jana kwamba upelelezi juu ya tukio hilo unaendelea.
Atakayebainika kutumia silaha kinyume cha taratibu, hatua itakayochukuliwa ni kunyang'anywa silaha na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria kama vile kupelekwa mahakamani.
Alisema sheria ya umiliki wa silaha hairuhusiwi kutishia maisha watu pasipo sababu za msingi na kuongeza kuwa vibali vya kumiliki silaha hutolewa kwa mtu mwenye akili timamu.
“Bado tunaendelea na upelelezi juu ya hilo na endapo ukweli utabainika basi mtu huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma,” alisema Kamanda Lutta.

No comments:

Post a Comment