Sep 11, 2012


Waandishi wa habari kuandamana leo,,


WAANDISHI wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, leo wanatarajia kufanya maandamano makubwa yenye lengo la kulaani mauaji ya mwenzao, Daud Mwangosi, aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo Iringa.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena alisema maandamano hayo yataanzia katika ofisi za Kituo cha Televisheni cha Channel Ten Mtaa wa Jamhuri na kuishia Viwanja vya Jangwani.

Meena

 alisema, maandamano hayo tayari yameruhusiwa na polisi na yatahusisha waandishi wote wa vyombo vya habari.

Meena alisema, katika maandamano hayo, waandishi wanatavaa nguo nyeusi au au watafunga vitambaa vyeusi mkononi ikiwa ni ishara ya kuuawa kwa mwandishi huyo.

Alisema maandamano hayo yatapokewa na viongozi wa TEF, na kisha waandishi wa habari waliokuwepo siku ya tukio watatoa ushuhuda wa kile kilichotokea na kufuatiwa na mjadala kuhusiana na mauaji hayo.

Mauaji ya Mwangosi ni ya kwanza kutokea nchini tangu taifa hili kupata uhuru wake mwaka 1961.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Heriet Komba, alithibitisha kuwepo kwa maandamano hayo na kueleza kuwa maandamano hayo yanabaraka za jeshi hilo.

“Ni kweli tumeruhusu maandamano kuanzia Channel Ten hadi Jangwani, ulinzi upo wa kutosha na askari wamejipanga hakuna tatizo,” alisema.

No comments:

Post a Comment