Sep 4, 2012

WARIOBA: TUTAPATA KATIBA MPYA APRIL 2014..

TUME ya Mabadiliko ya Katiba imejipanga kukamilisha majukumu ndani ya muda uliowekwa ili kupata Katiba Mpya ifikapo Aprili, 2014.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Joseph Warioba amewaeleza Mawaziri wa Katiba na Sheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa pamoja na changamoto zilizopo, dhamira hiyo ya Tume ipo palepale.

Mawaziri hao, Mathias Chikawe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Abubakar Khamis Bakari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walitembelea Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo na kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume hiyo.

“Tunafahamu hii ni changamoto, lakini tumeikubali na tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kama Taifa tunakuwa na Katiba Mpya ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014,” alisema Jaji Warioba katika mkutano mawaziri hao, ambao walitembelea vitengo vya Utafiti na Taarifa Rasmi (Hansard).

Jaji Warioba alisema kuwa lengo hilo la Tume linaongozwa na sababu kuu mbili ambazo ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambayo inaipa Tume muda wa miezi 18 kutekeleza majukumu yake. Tume hiyo ilianza kazi Mei mwaka huu (2012).

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, sababu ya pili ni hali ya kisiasa ilivyo hapa nchini, kuwa Taifa linahitaji kuwa na mwafaka wa kisiasa kupitia Katiba kabla ya mwaka 2015.

“Ukiangalia hali ya kisiasa, tunadhani itakuwa vizuri tukiwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki, Katibu wa Tume, Assaa Rashid na Naibu Katibu wa Tume, Casmir Kyuki.

Pamoja na nia hiyo, Jaji Warioba pia aliwaeleza mawaziri hao kuwa kwa sasa Tume yake imejikita katika kukusanya maoni binafsi ya wananchi na kuwa baada ya hatua hii, Tume itaanza kukusanya maoni ya makundi mbalimbali kama vyama vya siasa, taasisi za kidini, jumuiya za kitaaluma na asasi za kiraia.

Akizungumza katika mkutano huo, Chikawe alieleza kufurahishwa na utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.

“Kwa niaba ya Serikali napenda nikuhakikishie tena kuwa tutaendelea kuwapa kila aina ya ushirikiano mtakaouhitaji ili mtekeleze majukumu yenu kwa ufanisi,” alisema Waziri Chikawe.

Kwa upande wake, Abubakar Khamis Bakari aliwapongeza watendaji wa Sekretarieti hiyo kwa ubunifu

“Huu mfumo wa teknolojia wa kupokea na kuyafanyia kazi maoni ya wananchi ni mzuri na ingekuwa umetengenezwa na mtaalam kutoka nje, ingekuwa gharama kubwa,” alisema Waziri huyo wakati akizungumzia mfumo wa kompyuta uliotengenezwa na wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Tume hiyo.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba hivi sasa inaendelea na kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya kupitia mikutano katika mikoa saba ya Morogoro, Lindi, Katavi, Kigoma, Mwanza, Mbeya na Ruvuma.

Tayari Tume hiyo imekusanya maoni katika mikoa ya Tanga, Manyara, Kagera, Shinyanga, Dodoma, Pwani, Kusini Unguja na Kusini Pemba.

No comments:

Post a Comment