Dec 4, 2012

NAPE: VIGOGO CHADEMA WANA KADI ZA CCM,,,


*Wengine wanaendelea kuzilipia mpaka leo

*Ahoji Dk. Slaa kairudisha lini na wapi?
*Awaita waganga njaa si wanasiasa

MWANZA,TANZANIA
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, amerusha kombora kuwa vigogo wengi ndani ya CHADEMA wameendelea kuwa na kadi za CCM na wengine wanaendelea kuzilipia, jambo linalothibitisha unafiki walionao viongozi wengi wa upinzani nchini.

Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, leo uliokuwa na lengo la kupokea maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM na hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete, Nape amedai siasa kwa sasa imevamiwa na makanjanja wengi ambao kazi yao ni kuganga njaa na hivyo huishi kinafiki kwakuwa wakisemacho sicho wanachokiishi.

Sambamba na kombora hilo, Nape ameitaka CCM kuhakikisha inatoa uongozi mzuri ili kudhibiti uvamizi huu wa makanjanja kwenye siasa za hapa nchini.

"Siasa leo imevamiwa na makanjanja waganga njaa, ambao kwakweli wanachosema na wanachotenda ni vitu viwili tofauti, hawaishi maneno yao. Tunao viongozi wengi wa Chadema ambao kucha kutwa wanaishambulia CCM kwa maneno wakati tunawaona wakija kulipia kadi zao za CCM" alisema Nape.

"Kama nasema uongo, Babu Dk. Slaa  ajitokeze aseme kadi yake ya CCM aliirudisha lini na kumkabidhi nani. Lakini ninayo orodha ya vigogo kibao wa Chadema ambao huja kulipia kadi zao za CCM kila mara. Huu ni unafiki mkubwa" alisisitiza Nape.

Nape alisema kauli ya Dk. Slaa kudai kwamba anataka kukisafisha Chadema kwa madai kuwa kuna viongozi wa chama hicho ngazi za chini ambao ni mamluki waliopandikizwa na CCM, ni kuweweseka vibaya kwa kuwa wenye kadi za CCM si viongozi hao wadogo tu, hata vigogo wa juu kabisa wa Chadema wana kadi za CCM, hivyo awe makini asije kujikuta anajifukuza na yeye kwa kuwa hakumbuki ni lini alirudisha kadi ya CCM.

Kuhusu DK. Slaa kuitupia tuhuma mbalimbali sekretarite mpya ya CCM,  Nape anasema anamshangaa kushughulika na uongozi ndani ya CCM badala ya kujenga Chama chake ambako kinamsambarakitikia mikononi kila kukicha.

"Sana huyu Babu, hivi yeye badala ya kujenga chama chake ambacho kinamsambaratikia mikononi kila siku anaweweseka na sekretariete mpya ya CCM, nani kampa kazi ya kuitathimini sekretariti mpya ya CCM?" alishangaa Nape.

Nape aliwapongeza viongozi wa CCM wilaya ya Nyamagana kwa aina ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya wilaya waliyoitisha katika mkakati wa kuendeleza yale yaliyoamuliwa na mkutano mkuu wa CCM taifa.

"Palianza kujengeka utamaduni wa baada ya kufanya maamuzi kwenye vikao hakuna utaratibu wa ngazi za chini kuyachukua maamuzi na kuweka mkakati wa kuyatekeleza, nyie Nyamagana mmefungua ukurasa mpya, nawapongeza na kuagiza wilaya zote nchini na ngazi zingine za chama kuiga mfano huu mzuri wa Nyamagana" alisema Nape.

Aidha amesisitiza agizo la Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kuwa ni lazima kuitoa CCM ofisini na kuipeleka kwa watu kama njia ya kuwa karibu zaidi na watu na kujua matatizo yao na kisha kuyatafutia ufumbuzi.

"Nasisitiza viongozi wa ofisini hatuwataki kwa sasa, lazima kutekeleza kwa vitendo agizo la katibu mkuu la kutoka ofisini na kuipeleka CCM kwa watu, mtaani kuwasikiliza, kujua matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi." alisema Nape.

No comments:

Post a Comment