May 6, 2013

WIZI MTUPU! ... KULIONA KABURI LA KANUMBA SH. 5,000



KATIKA kile kinachoonekana kwamba ni wizi mtupu, baadhi ya vijana wanaojifanya kutunza Makaburi ya Kinondoni wamebuni njia ya kuwaibia watu kwa kutumia kaburi la nguli wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba.
Vijana hao hujipatia kipato kwa kuwatoza watu wanaofika makaburini hapo shilingi 5,000 kwa ajili ya kuliona na kupiga picha na kaburi la nguli huyo.



WAGENI WANALIZWA ZAIDI
Utafiti uliofanywa na Risasi Jumamosi umebaini kwamba wageni wanaotoka nje ya Dar ndiyo wanaoongoza kwa kulizwa zaidi.
Sosi wetu ambaye naye alilizwa, alisema kuwa alishangazwa kwa kutozwa fedha na vijana hao lakini hakuwa na budi kufanya hivyo yeye na wenzake ili kutimiza lengo la kulitembelea kaburi hilo la kipenzi chao.
Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili liliunda kikosi kazi cha waandishi wake na kwenda kuwanasa vijana hao.

WAANDISHI WATINGA MAKABURINI
Alhamisi iliyopita, waandishi wetu walifika katika Makaburi ya Kinondoni na kukutana na jamaa kibao waliokuwa wakijishughulisha na kazi za ujenzi wa makaburi na kupanda maua ambapo walimchagua mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Mdenmark ili kuongea na wageni nao.

WAPANGA DAU
Baada ya kuwaita chemba, jamaa huyo alianza kuwapiga somo waandishi wetu na kuwaambia kwa kuwasaidia wampe shilingi 5,000 ili kuwaonesha kaburi na kuwapa historia ya marehemu tangu enzi za uhai wake mpaka alipokutwa na umauti huku akiwatahadharisha wafanye jambo hili kuwa siri.

MCHEZO WAMALIZWA
Baada ya kukubaliana kiasi hicho cha fedha, waandishi walimpatia Mdenmark kiasi cha fedha na akachukua jukumu la kuwapeleka mahali lilipo kaburi hilo.
Wakiwa kaburini kwa Kanumba, waandishi wetu kwa kutumia ustadi mkubwa walifanikiwa kumpiga picha tapeli huyo akiwaelekeza mambo kadhaa juu ya marehemu na picha nyingine zikimuonesha akipokea fedha kutoka kwa waandishi.

TAMKO LA MHARIRI
Si sawa kulipa fedha kwa ajili ya kuliona kaburi la Kanumba, mara kadhaa waandishi wetu wamemsikia mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa akisema kuwa hafahamu mradi huo.
Ni jukumu la Jeshi la Polisi chini ya Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Suleiman Kova kuwanasa wajanja hao.

No comments:

Post a Comment